Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa, amesema chama hicho kimeshajiandaa vya kutosha kwa ajili
ya kufanya maandamano yatakayofanyika Septemba mosi.
Amesema kwamba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia nay a watu wote, haiwezekani mtu mmoja azuie demokrasia.
Lowassa aliyasema hayo jana mjini Tunduma, mkoani Songwe, alipokuwa
akizungumza na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa ndani
uliolenga kuweka mikakati ya kufanikisha kile wanachokiita Umoja wa
Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
“Ukuta siyo fujo, Ukuta siyo machafuko bali Ukuta unalenga kupiga
kelele dhidi ya uvunjwaji wa haki ya kidemokrasia na katiba ya nchi,
unaofanywa na utawala huu wa awamu ya tano.
“Hivi Chadema ni nani wakapambane na polisi ambao ni watoto wetu, ndugu zetu na hata wake na waume zetu?
“Ila tunawahakikishia hatutorudi nyuma pale katiba na haki ya kidemokrasia itakapochezewa au kuwa chini ya mtu fulani.
“Najua polisi watapiga watu, wataumiza watu na hata kuua, ila
niwahakikishie wao na walio na mamlaka wataishia katika mahakama ya
kimataifa,” alisema Lowassa.
Pamoja na msimamo huo, Lowassa ambaye aligombea urais kupitia Chadema
wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alisema chama chake bado kimefungua
milango ya mazungumzo kwa vyombo vinavyohusika kabla ya Septemba mosi.
“Milango yetu bado iko wazi kwa ajili ya mazungumzo ila kwa kuwa
hawahitaji, na sisi hatutorudi nyuma Septemba mosi kwa kuwa tumejiandaa
vya kutosha.
“Kwa sasa tuko ngazi ya kaya na nyinyi wajumbe mkakamilishe kazi
katika kaya zenu ili tarehe mosi sauti ya kutosha ipazwe kwa maandamano
na mikutano kama tulivyokubaliana katika kata zetu na majimbo nchi
nzima.
“Haiwezekani hata kidogo mtu mmoja azuie kila kitu, nchi hii ni mali
yetu sote. Kitendo cha Serikali ya awamu ya tano cha kupiga mafuruku
mikutano ya siasa ni uvunjwaji wa kanuni na katiba ya nchi, ibara ya 20
(1).
“Vilevile ni ukiukwaji wa sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11.
“Kwahiyo, eleweni kwamba Kamati Kuu yetu ilipoamua katika suala la
Ukuta haikukurupuka kwa sababu inaundwa na mchanganyiko wa wasomi wa
kada mbalimbali, wakiwamo wazee wenye busara na vijana machachari. Na
pia Ukuta ni haki ya Watanzania wote,” alisema.
Katika maelezo yake, Lowassa alitolea mfano kiongozi mmoja wa
Ujerumani aliyemtaja kwa jina la Martin Nimolar aliyejitokeza kupinga
ukandamizaji wa demokrasia wakati unaanza nchini humo.
“Kule Ujerumani wakati ufashisti unaanza, yupo mchungaji mmoja
aliyefahamika kwa jina la Martin Nimolar, ambaye alisema ‘at first they
came’ na na sisi tuna wimbo huu huu katika Ukuta.
“Awali walifungia matangazo ya Bunge ‘live’, hatukusema kwa kuwa sisi si wabunge, lakini sasa tunaamua kusema,” alisema.
Pamoja na hayo, mwanasiasa huyo aliwapa matumaini ya ushindi wa urais
mwaka 2020 wafuasi wa chama hicho kwa kusema uko wazi iwapo tu wataamua
kushikamana.
Alisema kwamba kama watakuwa na umoja, wakiheshimiana, wakisameheana
na kuimarisha chama ndani na nje ya chama pamoja na kwa wananchi, hakuna
kitakachokwamisha.
Pamoja na hayo, aliwashukuru wananchi wa Mbeya kwa kura walizompa
wakati wa uchaguzi mkuu na kuwataka wasikate tamaa kwa kuwa nafasi ya
ushindi bado ipo.
Awali, wakati anawasili mjini Tunduma, Lowassa alipokewa na mamia ya
wananchi na kusababisha baadhi ya biashara na huduma za kijamii
kufungwa.
Kutokana na wingi wa watu, askari polisi waliokuwa na silaha za moto,
walianza kuwatawanya, jambo ambalo lilisababisha vurugu zilizodumu kwa
dakika kadhaa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema , Mkoa wa Songwe, Jicva Jivava,
aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote waliyopewa kwa kuwa wako tayari
kuimarisha Ukuta.
Lowassa na timu yake, kesho wataendelea na ziara mkoani Katavi na Rukwa kwa ajili ya kuendelea na vikao vya ndani.
0 comments:
Post a Comment