Serikali imeazimia kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2018.
Maazimio hayo yamebainishwa na
Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama katika uzinduzi wa mafunzo ya
uanagenzi ya ushonaji nguo katika kiwanda cha Tanzania Tooku Garments
Company, Ltd.
Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa
katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kwamba ifikapo
mwaka 2018 soko la Afrika Mashariki halitaingiza nguo za mitumba kutoka
nje.
Ameongeza kuwa kwa kutekeleza
azimio hilo Serikali imeandaa mafunzo ya kuhakikisha vijana wengi
wanapata stadi za kushona nguo nchini ili kuwawezesha kufanya kazi
katika viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa kwa ajili ya kutengeneza
bidhaa zetu wenyewe na kuacha kutegemea bidhaa kutoka nje.
“Tumejipanga kutekeleza azimio
hili na kwa kushirikiana na kiwanda hiki tunategemea kutoa mafunzo ya
uanagenzi kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo,
kukata, kushona na kumalizia nguo” alisema Mhe. Jenista.
Aidha Waziri huyo amewapongeza
washiriki wa mafunzo hayo kwani mafunzo hayo yatawasaidia kuendana na
viwango vya soko la kimataifa na mahitaji ya soko la nguo kwa kutumia
teknolojia ya kisasa katika kubuni mitindo, kukata na kushona nguo zenye
ubora wa kimataifa.
“Imani yangu kuwa wataalamu
waliopo katika kiwanda hiki watawapa ujuzi wa kutosha na wengine
wataweza kupata ajira katika kiwanda hiki tumieni fursa hii mliyoipata
ni ya pekee kwani mmebahatika kuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza
kupata mafunzo chini ya Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini.
Mhe Jenista amesisitiza kuwa
mafunzo hayo yatawezesha vijana kupata ajira katika Viwanda, kujiajiri
na hata kutoa ajira kwa wengine hivyo vijana watumie fursa hiyo
kutengeneza mtaji na kujiunga katika vikundi vitakavyowawezesha
kufungua viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza nguo na kuendelea kukuza
ujuzi waliopata.
Pia Waziri Jenista ametoa wito kwa
viwanda vingine kushirikiana na Serikali kukuza ujuzi kwa vijana
kupitia mafunzo ya uanagenzi na kuwahakikisha kuwa Serikali itaendelea
kuwawezesha Vijana kupata mafunzo ya aina hiyo.
“Napenda niwahakikishie kuwa
Serikali iko bega kwa bega nanyi, fungueni viwanda vingi sehemu
mbalimbali katika nchi yetu, sisi kama Serikali tutashirikiana kwa
pamoja kuhakikisha rasilimali watu ya kuendesha viwanda hivi
inapatikana”
Mbali na hayo Serikali inayo
mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi
ya viwanda na kuwa na uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Serikali iliingia makubaliano na
kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd kutoa mafunzo ya uanagenzi
kwa vijana 2,000 kwa mwaka katika stadi za kubuni mitindo, kukata,
kushona na kumalizia nguo jumla ya vijana 1,089 waliomba nafasi ya
kupata mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa awamu tatu na kwa sasa jumla ya
vijana 430 wanapata mafunzo hayo.
0 comments:
Post a Comment