Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa mkoa wa Mbeya baada ya kupokea taarifa ya mkoa Agosti 7, 2016 kwenye Ikulu ndogo ya mbeya . Agosti 8, 2016 atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za wakulima Nanenane.
*Awataka wafanyabiashara kuwaripoti watendaji wanaoongeza kiwango kikubwa cha kodi kuliko inavyostahili kulipwa.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kuimarisha kitengo cha tathmini ili
kuweka viwango halali ambavyo havitawagandamiza wafanyabiashara na uwepo
uwazi kuhusu viwango stahili vya kodi wanavyotakiwa kulipa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
jioni (Jumapili, Agosti 07, 2016) wakati alipozungumza na viongozi wa
mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na Njombe mara
baada ya kuwasili mkoani Mbeya kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya
maonyesho ya nane nane kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
yanayofanyika mkoani Mbeya.
‘‘TRA waendelee kukusanya mapato
vizuri ila kuna wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati wa Serikali
kwa kufanya mambo ya hovyo kwa kuwaongezea viwango vikubwa vya kodi
kuliko kodi stahili wanavyotakiwa kulipa na kufanya suala hili liwe kama
tatizo au adhabu kwao jambo ambalo si sahihi. Naagiza watendaji wa TRA
wanaofanya hivyo wasakwe na wachukuliwe hatua“, alisema.
‘‘Wafanyabiashara mnaoonewa kwa
chuki binafsi na watendaji wa TRA toeni taarifa ili muweze kufanya
biashara zenu kwa uhakika bila ya wasiwasi lengo ni kuwafanya muweze
kulipa kodi sahihi kwa mujibu wa sheria“, alisema.
Ili kufanikisha mpango huo Waziri
Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwasikiliza wafanyabiashara
ambao wana malalamiko ya kweli ya kutotendewa haki katika kutozwa kodi
kwa sababu mchango kupitia kodi ni kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa
Taifa.
Katika hatua nyingine ameitaka
idara ya Uhamiaji ijikite katika kudhibiti watumishi wasiokuwa waaminifu
ambao wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwa wageni wanaotoka nje ya
nchi na kuwaingiza nchini bila ya kuwa na vibali maalumu.
‘‘Ni lazima tuhakikishe hakuna
uingiaji holela ndani ya nchi na hasa kwa wanaoingia bila vibali
maalumu kwani bila ya kudhibiti suala hilo tunaacha mianya ya kuingia
watu wasiokuwa na nia njema na Taifa letu. Watu watakaobainika wameingia
nchini bila ya vibali wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya
sheria,“ alisema.
Alisema kitendo cha mipaka
kushindwa kudhibitiwa na kuruhusu uingiaji holela wa watu wasiokuwa na
vibali chini kunasababisha Serikali kushindwa kuteleza ipasavyo mipango
yake ya kuwahudumia wananchi kulingana na idadi halisi.
Mbali na kuiagiza Idara ya
Uhamiaji pia Waziri Mkuu alisema wakuu wa mikoa ya mipakani wana jukumu
la ziada la kuhakikisha wanadhibiti mipaka yote na kuhakikisha hakuna
watu wanaoingia nchini bila ya kuwa na vibali.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka
wakuu wa mikoa kote nchini kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na
usalama katika maeneo yao na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani
na utulivu ili Watanzania waweze kutekeleza shughuli zao za maendeleo
kama walivyojipangia.
“Natambua kuwa wakuu wa mikoa na
wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika
maeneo yenu, endeleeni kuimarisha hali ya ulinzi na usalama. Nchi hii
tunahitaji iwe tulivu na salama na ni wajibu wenu kuhakikisha kwamba
lolote linalotokea mnalikabili vilivyo“, alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.
Makalla alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu alisema
mkoa huo una jumla ya viwanda 1,653 kati yake vikubwa ni tisa, vya kati
19 na vidogo 1,625 na bado wanaendelea kuzisimamia halmashauri kutenga
maeneo zaidi kwa ajili ya kuongeza na kupanua viwanda.
Mhe. Makalla alisema katika eneo
hilo la viwanda mkoa una kiwanda kimoja cha kusindika nyama cha
Tanganyika Pachers kilichopo wilayani Mbeya ambacho hakijawahi kufanya
kazi tangu kilipojengwa na kufungwa mitambo mwaka 1975.
Mkuu huyo wa mkoa alisema
usimamizi wa kiwanda hicho uko chini ya Masajili wa Hazina na kwamba
tayari kuna muwekezaji amepatikana kwa ajili ya kukiendesha hivyo
ameiomba Serikali kuharakisha taratibu za mikataba ili kiweze kuanza
kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment