Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
amewasimamisha kazi vigogo wawili wa Shirika la Ndege la Tanzania
(ATCL), kwa uzembe katika utendaji kazi ikiwamo kuteua watu
wasiokuwa na sifa ‘vilaza’ kwenda kwenye mafunzo ya urubani Canada.
Waliosimamishwa kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, i
Jonathan Mfinanga na Kapteni Sadicki Muze. Wote wanatuhumiwa kuteua
watu wasio na sifa kwenda Canada kwa mafunzo ya urubani wa ndege.
Akitoa agizo la kusimamishwa kazi kwa watendaji hao jana, Profesa
Makame alisema Serikali ipo katika mchakato wa kununua ndege mbili.
Hivyo kabla ya kuwasili ndege hizo ni vema baadhi ya wataalamu wakapelekwa Canada kupata mafunzo, alisema.
Alisema Serikali imekwisha kulipia Dola za Marekani bilioni 40 na
kwamba ifikapo September 14, mwaka huu ndege hizo zitakuwa zimewasilia
nchini.
Waziri alisema kwa sababu hiyo, ni vema ATCL ikaandaa marubaini wake kwa ajili ya kurusha ndege hizo.
“Marubani wanaotakiwa ni wanne lakini awali nililetewa majina ya
marubani tisa ambao baadhi yao waliondolewa kutokana na kukosa sifa.
“Lakini orodha ya majina iliyobaki ililetwa kwangu kwa ajili ya
kuipitia na niliwauliza wahusika kwamba mna uhakika na hawa watu?
Wakaniambia ndiyo tuna uhakika nao.
“…niliwauliza kwa mara ya pili mna uhakika na haya majina mlioniletea wao wakaniambia ndiyo mkuu.
“Sasa leo (jana) asubuhi naletewa taarifa kwamba kuna tatizo
limejitokeza kwa wale watu watano wanaotakiwa kuondoka kesho (leo)
kwenda Canada kwa ajili ya mafunzo ya ndege yanayoanza Agosti 8, mwaka
huu,” alisema.
Alisema licha ya kutoa agizo la kuteuliwa watu wenye uwezo, bado
watendaji hao wamefanya uzembe na kuteua watu ambao hawana sifa za
urubani ‘vilaza’.
“Wamechagua marubani lakini kidogo mchakato haukwenda vizuri, kwa
kuwa na mimi nilitoa maelekezo nikasema hapana hivi sasa kwenye
shirika la ndege ama mashirika yote watu lazima wawe na nidhamu
wakifanya kitu lazima kiwe na uhakika.
“Nimeletewa ripoti ile asubuhi kwamba kuna tatizo limejitokeza nikawaambia kila aliyesababisha tatizo hilo awajibike,” alisema.
Alisema katika marubani watano ambao serikali ilikuwa ikiwapeleka
nje kujifunza mmoja ‘kilaza’ amekutwa na kasoro ambazo hazikidhi vigezo
vya urubani.
“ Leo (jana) nimepigiwa simu na mtu, halafu nikajihakikishia upande
mwingine nikaambiwa kuna tatizo na kwamba hatuwezi kulitatua kwa vile
wale marubani wanatakiwa kusafiri kesho (leo).
“Hivyo tukianza mambo mengine itatuchelewesha na kozi inaanza Agosti
8. Sasa nikawaambia wale waliohusika na uzembe hata kama ni kidogo
hatuwezi kukubali ni lazima wasimamishwe kazi mara moja,”alisema.
Alisema mtu wa kwanza ni Jonathan Mfinanga, ambaye alikuwa Kaimu
Mkurugenzi wa ATCL na Kapteni Sadick Muze ambaye ni Mkurugenzi wa
Operesheni na Uendeshaji.
“Watu hawa wawili ni lazima wachukue dhamana, hatuwezi kuendelea na
mtu anafanya jambo la kizembezembe halafu akaachwa wakati niliwaita mara
mbilimbili na nikatoa maelekezo lakini bado wamefanya wanavyojua
wao,”alisema.
Waziri alisema amekwisha kutoa maelekezo atafutwe mtu mwingine
atakayekaimu nafasi hizo na Serilikali inaendelea na utatuzi wa suala
lililojitokeza huku marubani waliotakiwa wakitarajiwa kuondoka leo.
0 comments:
Post a Comment