Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa
na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa Habari
(hawapo Pichani) kuhusu mchezo kati ya Serengeti Boys na
Congo-Brazaville utakaofanyika Septemba 18 katika Uwanja wa Taifa Jijini
Dar es Salaam. Picha na May Simba WHUSM
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa
na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye ameahidi kutoa shilingi laki tano kwa
kila goli litakalofungwa na timu ya Serengeti Boys katika mchezo wa
kuwania kufuzu fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya
umri wa miaka 17 utakaofanyika kesho katika Uwanja wa Taifa dhidi ya
Congo-Brazzaville.
Akiongea na waandishi wa habari
leo Jijini Dar es Salaam Mhe.Nape amesema milango ipo wazi kwa wadau
wengine wa michezo kujitolea katika kuiwezesha timu na hivyo kufanya
vizuri katika mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda ili kufuzu kwa
fainali hizo.
“Hii timu ni yetu sote hivyo
inahitajika tuimiliki, tuepe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na
hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville”
alisema Mhe. Nape.
Aidha aliongeza kuwa kesho asubuhi
atakutana na wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla
ya kuanza kwa mechi na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi
uwanjani ili kuwapa motisha wachezaji kwa kuwashangilia na kuwatia
moyo.
Mbali na hayo Waziri Nape alitoa
ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za kieletroniki zilizozinduliwa hivi
karibuni kwa kueleza kuwa kadi hizo bado hazijaanza kutumika rasmi ili
zitaanza kutumiwa katika mchezo baina ya Wabunge wa Simba na Yanga
pamoja na Bongo Fleva.
Timu ya Serengeti Boys inaundwa na
vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo
wa kesho watahitaji ushindi na baadaye kufanya mechi ya marudiano mnamo
Oktoba 2 mwaka huu nchini Congo-Brazzaville.
0 comments:
Post a Comment