Stara Sudi, mke wa Saidi Mrisho ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
jinsi alivyoshtuka baada ya kupokea simu aliyopiga mumewe kuwa amevamiwa
na kuchomwa visu machoni, mgongoni na tumboni.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga kutoa ushahidi dhidi ya
mshtakiwa Salum Njwete (34) maarufu ‘Scropion’, Stara alimueleza Hakimu
Mkazi, Flora Haule kuwa Septemba 6, saa tano usiku akiwa amelala
alipokea simu yenye sauti ya mumewe ikieleza kuwa amevamiwa.
“Aliniambia mama Nancy nimechomwa visu hata kuona sioni hapa nilipo nipo
Buguruni,” alidai Stara ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa
mashtaka.
Alidai tangu wafunge ndoa na mumewe Oktoba 2015 , Said alikuwa akifanya
kazi ya kinyozi katika saluni ya Rodgers iliyopo Tabata Sanene.
“Baada ya kuongea na mume wangu, simu ilikatika lakini wakati natafuta
nguo nivae simu ileile ilipiga na nilipopokea sauti ya mtu mwingine
iliongea ambaye ndiye mwenye simu na aliniambia kuwa mume wangu ana hali
mbaya hivyo nifanye haraka niende Hospitali ya Amana,” alidai Stara.
Baada ya kupata taarifa hizo, alidai alimweleza mtoto wao mkubwa, Abdul
Said (12) kuwa anaelekea Amana. Lakini kabla ya kwenda huko alichukua
pikipiki na kwenda Mabibo Hosteli anakoishi mama mkwe wake kumweleza
taarifa hiyo na kwamba waliambatana hadi Amana.
Alidai wakiwa njiani, walimjulisha mdogo wa Saidi, Yahaya Kisukari (23)
kuwa kaka yako amepata matatizo ya kuvamiwa na mtu akachomwa visu na
yupo Hospitali ya Amana.
“Tulipofika Amana, tuliruhusiwa kuingia wodini na kumuona mume wangu
akiwa amefungwa bandeji machoni na sehemu nyingine za mwili, huku damu
ikivuja sehemu mbalimbali za mwili. Hata nguo aliyovaa ilikuwa imejaa
damu,” aliiambia Mahakama na kuongeza: “Baada ya kumvua nguo zilizo-
kuwa zimetapakaa damu, tulipewa rufaa kwenda Muhimbili kwa ajili ya
matibabu na wakati huo ilikuwa imeshafika saa sita usiku.”
Stara alidai baada ya kumuona mumewe aliyechomwa visu na mtu aliyemtaja
kwa jina la Scorpion, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi
Buguruni.
“Baada ya kutoa maelezo Polisi Buguruni na askari kwenda kuchukua
maelezo ya mume wangu Muhimbili, tulikwenda kumkamata mshtakiwa Salum
Njwete,” alidai.
Alidai: “Septemba 8, tulirudi tena Muhimbili na kupewa taarifa na
daktari wa macho aliyemfanyia upasuaji Said kuwa macho yake hayataona
tena.” Stara alidai tangu waoane na mumewe, hajawahi kupata malalamiko
yoyote kuwa mwenza wake huyo ni mwizi.
0 comments:
Post a Comment