Meneja wa klabu bingwa nchini England Leicester City Claudio Ranieri,
amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kufanya kazi na uongozi wa
klabu hiyo hadi mwaka 2020.
Ranieri amejitia kitanzi kwa kusaini mkataba huo, kufuatia mafanikio
aliyoyavuna klabuni hapo msimu uliopita, ambapo aliiwezesha Leicester
City kutwaa ubingwa wake wa kwanza katika historia ya soka ya soka
nchini England.
Baada ya kukamilisha mpango huo, meneja huyo kutoka nchini Italia
alisema imekua faraja kwake kuendelea kubaki klabuni hapo tena kwa nguvu
ya viongozi ambao wameonyesha kukunwa na mafanikio aliyowaletea msimu
uliopita.
“Nilizungumza na uongozi na umeniambia nini mustakabali wa Leicester
City kwa siku za usoni, hivyo ninajua nimefanya maamuzi sahihi ya
kuendelea kubaki klabuni hapa.
“Natumai mambo mazuri yataendelea kupatikana kwa ushirikiano na
viongozi wangu ambao wameonyesha kuwa bega kwa bega nami, hivyo sina
wasiwasi wa kuendelea kufanya kazi kwa lengo la kutafuta mafanikio
mengine kwa kipindi cha miaka minne kama mkataba wangu unavyoelekeza.”
Ranieli amenukuliwa na tovuti ya klabu ya Leicester City.
Meneja huyo mwenye umri wa miaka 64, alibadilisha mawazo ya mashabiki
walio wengi duniani kote baada ya kushindwa kupewa nafasi ya kufanya
vyema alipotangazwa kuwa meneja wa Leicester City mwanzoni mwa msimu
uliopita, kutokana na klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya 14 kwenye
msimamo wa ligi ya nchini England msimu wa 2014/15.
Kwa upande wa makamu mwenyekiti wa Leicester City Aiyawatt
Srivaddhanaprabha ameongeza kuwa: “Miaka 12 iliyopita, tulimtambulisha
Ranieri kwa waandishi wa habari na tulitambua uwezo wake, tulijiamini na
kuwapuuza waliotubeza kwa maamuzi yetu, na mwishoni mwa msimu uliopita
ilidhihiri nini tulichokua tumekitarajia.” Tovuti ya Leicester City
imeandika.
Leicester City (The Foxes) wanatarajia kushiriki kwa mara ya kwanza
michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2016/17 na huenda
wapangwa na timu za Borussia Dortmund, Atletico Madrid pamoja na
Sevilla.
Matarajio hayo yanatokana na kanuni mpya za upangaji wa makundi ya
michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambapo mabingwa wa nchi
husika hupangwa katika chungu A (Pot 1), hatua ambayo inawatenganisha na
mabingwa wa nchi nyingine kama FC Barcelona, Bayern Munich pamoja
na Real Madrid.
0 comments:
Post a Comment