Kampeni imezuka nchini Misri dhidi ya desturi ya kuwazawadia mabibi harusi dhahabu chungu nzima wakati wa harusi zao.
Mabwana harusi watarajiwa ambao hawana mali za kuwazawadia wapenzi wao wanasema desturi hiyo ni ghali mno.
Mbali
na mahari nyenginezo familia ya bwana harusi hutarajiwa kutoa kile
kinachoitwa kwa lugha ya kiarabu "shabka" ambayo ni dhahabu na vito
vyenginevyo vyenye thamani na wingi wa vyombo hivyo huonekana kama
kipimo cha hadhi ya familia hiyo na vilevile jinsi wanavyomthamini bibi
harusi huyo.
Lakini tatizo ni kuwa bei ya dhahabu inazidi kuongezeka kila uchao.
Kwa sasa gramu moja ya dhahabu ya carat 21-ni pauni za Misri 445 sawa na dola $50.
Bwana harusi huyo pia anatarajiwa kununua nyumba mbali na kulipa mahari ya bi harusi.
Sasa kampeni hiyo inayonuiwa kupunguza gharama za ndoa za Misri inazidi kuungwa mkono.
Katika hotuba ya ijumaa kwa wakaazi wa kijiji kimoja katika jimbo
liitwalo Qena kazkazini mwa nchi hiyo, wito umetolea maharusi waache
kupeana na kupokea zawadi za dhahabu na badala yake watoe zawadi
nyenginezo zenye hadhi lakini zisizo ghali.
Ni ujumbe ulioenea kwenye mitandao ya kijamii na tovuti za magazeti kama vile al-Watan.
Wengine
kupitia hashtag #Bride's_gift_silver wamependekeza badala ya dhahabu,
fedha ndio itumike zaidi kwani bei yake iko chini kidogo.
Waimbaji
pia wamejiunga na kampeni hiyo kama vile mwimbaji mashuhuri Amir Teima
ambae katika akaunti yake ya facebook anawataka wanandoa ‘mke na mume
wafanye kazi kwa bidii na kujenga msingi imara wa familia yao changa
badala
ya kutegemea zawadi tu kutoka kwa familia ya mume kwani ‘’harusi si bidhaa wala biashara.’ Amesema.
Viongozi
wa kidini kwa upande wao wameunga mkono jambo hilo wakisema
litawasaidia wanaotaka kuoa na vilevile kuondoa vishawishi kwa vijana
kujiingiza kwenye mapenzi ya nje ya ndoa.
Hata hivyo baadhi ya
wanawake wanasema ni utamaduni unaopaswa kudumishwa kwani dhahabu ni
sehemu muhimu ya mahari na ni haki bi harusi atuzwe na kuzawadiwa
inavyostahili .
0 comments:
Post a Comment