Na Abushehe Nondo (MAELEZO).
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema kuwa bado inaendelea kupokea maoni
kutoka kwa wadau mbalimbali wa usafiri wa treni inayofanya safari zake
kati ya Stesheni na Pugu jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja
Mawasiliano wa SUMATRA, Bw. David Mziray ambaye alibainisha kuwa kwa
sasa bado wanaendela kupokea maoni kutoka kwa wadau kama sheria ya
mamlaka hiyo inavyoelekeza kabla ya kuja na kiwango rasmi cha nauli ya
usafiri huo.
“Tumetoa muda mpaka Agosti 19
mwaka huu iwe ndio mwisho wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali
kuhusiana na bei elekezi ya nauli kwa treni inayofanya safari zake kati
ya Stesheni na Pugu” Alisema Mziray.
Pia, Mziray alifafanua kuwa kwa
kipindi hiki ambacho wanapokea maoni wameielekeza Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL) waendelee kutoza nauli ya shilingi 400 kwa watu wazima na
shilingi 200 kwa watoto na wanafunzi mpaka hapo itakapoamuliwa
vinginevyo.
Alieleza kuwa tangu usafiri huo wa
treni uanze huduma zake imeonekana kuwapunguzia wananchi adha ya
kusafiri muda mrefu njiani na sasa wanaweza kuwahi katika maeneo yao ya
kazi na biashara wakiwemo wanaokwenda kwenye soko la Kimataifa la samaki
la Ferry.
Aidha, aliongeza kuwa ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya usafiri pasipo na matatizo
yoyote kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajia kuongeza mabehewa
kutoka 15 yaliyopo sasa hadi kufikia mabehewa 20.
Akizungumzia baadhi ya changamoto
walizoziona tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo ya usafiri wa Treni alisema
kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma ya vyoo na maji katika baadhi ya
vituo.
“Tunatarajia hivi karibuni Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL) itajenga vituo vipya na kufanya ukarabati kwenye
vituo vya zamani ili kuweza kuwaondolea usumbufu wananchi kwa kuweka
huduma mbalimbali ikiwemo vyoo na maji kwenye vituo hivyo” Alisema
Mziray.
Treni ya Kampuni ya Reli Tanzania
(TRL) inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu ilizinduliwa hivi
karibuni na Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa na imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam
hasa wakazi wa maeneo ya Gongolamboto, Pugu na Chanika.
0 comments:
Post a Comment