Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekishauri Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kusitisha maandamano yake ili
kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo
la muda kati ya sasa na Septemba mosi mwaka huu.
Aidha, imelishauri jeshi la Polisi kutotumia neno ‘tutawashughulikia
wote watakaokaidi amri’ kwa kuwa imeona maneno hayo yanaweza kusababisha
matumizi mabaya ya mamlaka ya jeshi hilo.
Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu imetupilia mbali maombi ya
wadhamini wa Chadema ya kupinga amri iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu ya kupiga marufuku mikutano
ya kisiasa kwa muda usiojulikana.
Mwenyekiti wa THBUB, Bahame Nyanduga aliyasema hayo jana Dar es
Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa
mkutano uliohudhuriwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na washauri
wake pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania
(TCD), Daniel Loya.
Nyanduga alisema Tume iliandaa mkutano huo ili kuzungumzia tamko la
jeshi la Polisi la Juni 7, mwaka huu la kuzuia mikutano na maandamano ya
vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji na tamko la Chadema kuhusu
Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA) na
mikutano wanayopanga kufanya Septemba mosi, mwaka huu.
Alisema mkutano huo wa jana ulikuwa na lengo la kuwakutanisha
viongozi wa Serikali, jeshi la Polisi na Chadema na kwa pamoja kutafuta
ufumbuzi wa kile Tume inachohofia kuhusu uvunjifu wa amani, haki za
binadamu na utawala bora.
Aidha, alisema baada ya tamko la Chadema la kufanya maandamano nchi
nzima, kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kitaifa,
baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya, makamanda wa mikoa wa jeshi la
Polisi kukataza kufanyika kwa maandamano hayo na kwamba watakaokiuka
zuio hilo ‘watashughulikiwa.’
“Ni katika mazingira haya, Tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko
haya yataachwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu
mkubwa wa haki za binadamu unaoweza kutokea. Mkutano huo ulitaka
kujihakikishia iwapo Tume ina mamlaka ya kujadili hoja hizo mbili za
zuio la maandamano na mikutano ya vyama vya siasa visivyokuwa vya
kiutendaji na kuhusu lugha na matamshi yasiyostahiki,” alisema Nyanduga
.
Alisema baada ya majadiliano hayo, wajumbe wote waliohudhuria kikao
hicho walikubaliana kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini na umuhimu
wa kuwepo majadiliano katika kutafuta maafikiano ya tofauti zozote kila
mara zinapojitokeza na walipendekeza umuhimu wa kuendelea na majadiliano
yaliyoanzishwa na Tume.
“Kuhusu mustakabali wa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa
ilibainika kuwa kuna kesi mbili zilizofunguliwa na Chadema katika
Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam na Mwanza na kesi zote
zinaendelea. Kwa kuzingatia Ibara ya 131(2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, 1977 inaamini kwamba tafsiri sahihi ya zuio
lililotolewa na polisi litapatikana mahakamani,” alisema Mwenyekiti huyo
wa Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu.
Alisema Tume inaamini kwamba Mahakama itayapa mashauri hayo
kipaumbele kama ilivyofanya wakati wa kusikiliza kesi ya mita 200 Oktoba
mwaka jana ili tafsiri yake ipatikane mapema.
Alisema pamoja na uamuzi huo, kwa kuzingatia mamlaka ya Tume chini ya
Ibara 130(1)(g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu kutoa ushauri na
kutafuta maelewano kati ya viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi kwa
upande mmoja na uongozi wa Chadema, Tume imewaasa viongozi wa pande hizo
kuacha maneno yanayoashiria uvunjifu wa amani.
“Tunawashauri kusitisha matumzi ya lugha au maneno yenye viashiria
vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora kwani lugha hizo
hazikidhi matakwa ya haki za binadamu, wala utawala wa sheria,”
alieleza Nyanduga.
Aidha, alisema tayari kuna mashauri mawili yaliyopo mahakamani ambayo
yatawezesha Mahakama kutoa tafsiri ya uhalali wa zuio la Jeshi la
Polisi la Juni 7, mwaka huu kuhusu maandamano na mikutano ya vyama vya
siasa.
“Tume inashauri kwamba pande zote mbili ziheshimu Mahakama na ziache
kutoa matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto kuhusu uwepo au
kutokuwepo maandamano na mikutano Septemba mosi mwaka huu,” alifafanua.
Pia aliwashauri Chadema kurekebisha msamiati wa mikutano wanayopanga
na kuondoa neno ‘Udikteta’ katika mikakati yao ya kisiasa, kwani
Tanzania ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu utawala wa
sheria na ndiyo sababu Chadema wamekwenda mahakamani.
“Iwapo ushauri huu hautazingatiwa, Tume inatahadharisha kwamba kuna
uwezekano mkubwa wa kuwepo na uvunjifu wa haki za binadamu na iwapo
itatokea hivyo wahusika wote pia itabidi wawajibike,” alionya.
Hata hivyo, alipoulizwa baadhi ya wajumbe muhimu kutokuwepo katika
mkutano huo, Mwenyekiti huyo alisema wote walipewa taarifa ila Polisi na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walitoa taarifa kwa nini
wameshindwa kufika kwenye mkutano huo.
“Pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) walialikwa lakini hawakufika, hivyo
wao na wengine ambao hawakufika mnaweza kuwahoji nyie kwanini
hawakufika,” alisema.
Katika Mahakama Kuu, Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali alikataa maombi
ya wadhamini hao wa Chadema baada ya kukubaliana na hoja za kupinga
zilizowasilishwa na IGP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na kutetewa
kortini hapo na Mwanasheria Mkuu Mwandamizi, Gabriel Malata na
Mwanasheria Mwandamizi, Haruni Matagane.
Katika pingamizi zao, IGP na AG walieleza kuwa maombi yanayoombwa na
walalamikaji hayakuwa yamekamilika na kinyume cha sheria kwa kushindwa
kwa Wadhamini wa Chadema kufuata taratibu nyingine zilizopo kabla ya
kufungua kesi mahakamani.
Katika uamuzi wake, Jaji Kiongozi alibainisha kwamba walalamikaji
walikuwa na fursa ya kufuata taratibu nyingine, kwa kupeleka malalamiko
yao dhidi ya IGP kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kabla ya kwenda
kuomba zuio la mahakama. Alisema fursa hizo zinapaswa kufuatwa kwanza
kabla ya kuomba mahakama iingilie kati.
0 comments:
Post a Comment