Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Waziri Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali zote za Rufaa
nchini ngazi ya Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa
Matibabu Bure kwa Wagonjwa wa Fistula.
Waziri Ummy aliyasema hayo mjini
Tanga kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo katika uzinduzi wa
kambi ya matibabu ya Wagonjwa wa Fistula itakayodumu kwa kipindi cha
wiki moja kuanzia tarehe 15 hadi 19 agosti,2016.
Alisema tatizo la Fistula
limekuwa likiongezeka kila siku na waathirika wengi ni akina mama wa
vijijini na wale wa kipato cha chini ambao wanashindwa kupata huduma
sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma
za afya wakati wa kujifungua.
Takribani kina mama 2500 hadi
3000 hupata tatizo la ugonjwa wa Fistula kila mwaka japo idadi hii ni
ndogo sana kuliko hali halisi ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi
hunyanyapaliwa na familia zao na jamii kwa ujumla.
“Serikali ya Awamu ya Tano
imejikita zaidi katika kuwahudumia Wanyonge, kwa mamlaka niliyopewa
natoa msamaha wa kulipia matibabu ya Fistula ili kuwapunguzia mateso
wanawake hawa”.”Kwa kuwa wenye tatizo la Fistula ni wanawake wa kipato
cha chini na wa vijijini naziagiza Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na
Kanda kutoa Matibabu ya Fistula Bure kwa Wagonjwa watakaofika kutaka
Huduma hizo.”
Waziri Ummy alisema ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa ameziaagiza hospitali hizo kuandaa Kambi za Matibabu ya Fistula angalau mara moja kila mwaka na apatiwe Taarifa.
Aidha ,ameeleza kuwa kina mama
wengi wenye tatizo la Fistula wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za
uchumi kama biashara ndogo ndogo kwa kuwa ugonjwa huu ni wa aibu ambao
hupelekea watu kunyanyapaliwa na jamii.
Akieleza hatua mbalimbali
zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana tatizo la ugonjwa huu
ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za
ujauzito na uzazi, mafunzo ya huduma za dharura za uzazi kwa watoa
huduma za afya pamoja na usimamizi shirikishi, uimarishaji wa ubora wa
huduma za ujauzito na uzazi,kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
kwa ajili ya ujauzito na uzazi,kuimarisha mifumo ya rufaa na
kuhakikisha huduma za dharura za uzazi zinapatikana hasa maeneo ya
vijijini na wataalam waliobobea katika maeneo hayo.
“Utaratibu huu wa kushirikiana na
wadau na marafiki zetu ni Mzuri, kwani unasaidia kuongeza ujuzi kwa
wataalam wakiwa katika maeneo yao ya kazi. Pia,amewaomba wadau hao
kuongeza wigo wa ushirikiano katika eneo la Afya ya Uzazi ikiwemo
matibabu ya Saratani ya Shingo ya Kizazi”alisema Waziri Ummy.
Kuhusu uhaba wa watumishi katika
hospitali hiyo ya Rufaa,Waziri Ummy ameahidi kupanga watumishi
wanaohitajika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa pindi kibali cha ajira
kitakapotoka,Vile vile kutoa kipaumbele cha ufadhili wa masomo ya juu
kwa madaktari watakaoomba kuchukuwa masomo yatakayowawezesha kubobea
kwenye magonjwa ya akina mama na watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Tanga Dkt. Asha Mahita,alieleza kuwa hospitali ya Bombo ina
changamoto ya kuwa na miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa tiba na
watumishi kiasi ambacho wanashindwa kutoa huduma ya kutibu akina mama
wenye tatizo la Fistula kwa kuwa hawana wataalam waliobobea katika
maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa The Sunshine
Muslim Volunteers (SMV) Tanzania Dkt Juma Mwimbe alisema wameguswa na
tatizo la fistula kwa kuwa linawakumba wanawake maskini na wa hali ya
chini. Hivyo wataendelea kujitolea kwa kufanya kambi kama hizi kadri
watakavyoweza ili waweze kuwafikia kina mama wengi zaidi hasa wa
vijijini.
Kambi hii ya wiki moja inatarajia
kuhudumia kina mama wapatao 100 kutoka Mikoa wa Tanga na Manyara ambapo
wameweza kupatikana madaktari bingwa 7 kutoka nchi za Afrika Kusini,
Pakistani, Australia na Uingereza
0 comments:
Post a Comment