Dkt H. Mwakyembe Waziri wa Katiba
na Sheria leo amezungumza maalum na TBC1 kuhusiana na kauli ya jeshi la
Polisi . TBC1 walifika kupata ufafanuzi juu ya uhalali wa kauli ya
kuzuia mikutano iliyotolewa na jeshi la polisi jana.
Waziri wa Mambo ya Katiba na
Sheria Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amesema amri ya Jeshi la Polisi ya
kuzuia mikutano ya nje na ndani ya vyama vya siasa ni halali ambayo kila
Mtanzania na mwanachama wa chama chochote cha siasa anapaswa kuitii na
kuizingatia na kwamba kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.
Amesema amri hiyo ni ya kudumu
ambayo imelenga kuangalia na kufanya tathmini ya hali ya nchi kutokana
na viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa amani nchini ambavyo vimeanza
kuonekana.
Dkt Mwakyembe alikuwa akijibu
swali kutoka kwa Kituo cha Televisheni cha Taifa TBC 1 ambacho kilitaka
kupata ufafanuzi kuhusiana na uhalali wa kauli ya Jeshi la Polisi ya
kuzuia mikutano ya ndani na ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.
“Jeshi la Polisi ni chombo halali
cha cha dola kilichoanzishwa kisheria chenye wajibu wa kulinda usalama
wa raia na mali zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
kuongeza kuwa uamuzi huo una lengo la kulinda amani ya nchi na endapo
kutakuwa na viashiria vya kutishia amani ya nchi yetu lazima hatua za
kisheria na kinidhamu zichukuliwe. Ni amri halali na kila Mtanzania na
mwanachama wa chama chochote nchini anapaswa kuitii na kuizingatia na
kwamba kwenda kinyume ni kukiuka sheria, ” alisisitiza Mhe. Mwakyembe.
Mhe. Waziri amesema ni haki ya
vyama vya siasa kufanya mikutano ila wanatakiwa kutoa taarifa Polisi ili
waweze kutoa ulinzi wakati wa mkutano huo na kuongeza kuwa Jeshi la
Polisi linaweza kuzuia mikutano hiyo kwa sababu za kiusalama.
Mhe. Waziri pia alisema sio kweli
kuwa Mhe. Rais amezuia mikutano ya siasa, bali alichofanya ni kudhibiti
uendeshaji wa holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya
uchaguzi ya wanasiasa na kuongeza kuwa Mhe. Rais amefanya hivyo kutokana
na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.
“Mhe. Rais hajapiga marufuku
siasa, alichofanya ni kudhibiti uendeshaji holela au huria wa shughuli
za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa husika kuepusha shari na
chuki na amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda,
kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Tanzania na taifa kwa ujumla wake. Kwa
hatua hiyo Mhe. Rais hajafunga milango ya majadiliano. Milango iko wazi
na tulitegemea wenzetu wangekuja na njia mbadala na kulizungumzia hilo
badala ya kuitisha maandamano ya nchi nzima, alisema.
Mhe Mhe. Waziri amevitaka vyama
vya upinzani nchini kukaa na kuzungumza na Serikali na kuacha kufanya
vitendo vya kutishia uvunjifu wa amani kama kuitisha maandamano kwa nchi
nzima. “Njooni tukae tuzungumze tupime ushauri wenu, hili ni taifa letu
sote na milango iko wazi, tuache kuchochea vitendo vya uvunjifu wa
amani kama ambavyo inavyoonekana nchini hivi sasa,” alisisitiza.
Amasema Sheria ya Vyama vya siasa
hairuhusu kufanyika kwa maandamano kwa nchi nzima, kufanya hivyo ni
kuchochea wananchi kuasi “civil disobedience” ni kinyume cha sheria na
serikali haiwezi kuivumilia hali hiyo. Mhe. Waziri ametoa wito kwa
Watanzania wote kutoshiriki maandamano ya Ukuta ambayo alisema
hayatakuwa na tija kwa nchi bali kuleta vurugu katika jamii.
0 comments:
Post a Comment