TANGOZO

TANGOZO
Latest News
Tuesday, September 13, 2016

NIDA KUANZA KUTOA VITAMBULISHO VIPYA WIKI HII

Mfano wa kitambulisho kipya chenye saini.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe; utekelezaji wa zoezi hilo utaanza rasmi siku ya Jumatano wiki hii katika ofisi zote za NIDA zikiwemo ofisi za wilaya zilizoanza usajili Tanzania Zanzibar na mikoa ya Dar-es-Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma pamoja na waheshimiwa Wabunge Dodoma.

Amefafanua kwamba, waombaji wote ambao vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu zao za mkononi kufahamishwa kufika katika vituo vya usajili kuchukua vitambulisho vyao.

Kuhusu wananchi ambao tayari wana vitambulisho visivyo na saini; Bw. Massawe amesema…. “ Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani visivyo na saini, ila kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika sambamba na vipya wakati taratibu za kuendelea kuvibadilisha zikiendelea” alisisitiza.

Amesema kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalum kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji (chip); ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika katika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.

Akizungumzia wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa, Bw. Massawe amesisitiza kwamba wananchi wote ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea; kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, kuendelea kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kupata vitambulisho vya taifa kwani zoezi la usajili ni endelevu.

“ Kwa wale wananchi ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Mpiga kura NEC; NIDA iko mbioni kuanza kutoa nambari za utambulisho wakati tukiendelea kukamilisha taratibu za usajili ili kupata utambulisho kamili na kuanza kunufaika na matumizi mapana ya utambulisho wa taifa wakati taratibu za uzalishaji wa vitambulisho zikiendelea”.

Wananchi wanakumbushwa kutunza vizuri vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji akilipie.

Kwa sasa vitambulisho vya taifa vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma nchini hususani kwenye mabenki kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupatiwa huduma.

Taratibu za kupanua wigo wa matumizi ya vitambulisho kielektroniki kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, zinaendelea.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Post a Comment

Item Reviewed: NIDA KUANZA KUTOA VITAMBULISHO VIPYA WIKI HII Rating: 5 Reviewed By: SIMAMA BUKOBA