Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi
Wilaya ya Kaskazini “B” kichama wameshauriwa kujiandaa kisaikolojia
kuwania nafasi za uongozi katika Uchaguzi ujao wa CCM ili kupata
viongozi bora watakaokuwa na uwezo na weledi wa kiutendaji
Akizungumza kwa nyakati tofauti
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar,
Waride Bakar Jabu katika ziara ya kuimarisha Chama huko katika Matawi
ya Bubwini Mafufuni na Donge Kitaruni.
Alisema maandalizi yakifanyika
mapema kwa kutoa taarifa mbali mbali kwa watu wenye nia na sifa za
kugombea uongozi zinazokubalika ndani ya CCM itasaidia kuwapata viongozi
wazuri na waliokomaa kisiasa.
Alieleza kwamba suala la
kujiandaa kuwa kiongozi ndani ya Chama hicho linatakiwa kwenda sambamba
na kujitathimini hali ya kisiasa iliyopo ndani na nje ya chama hicho kwa
lengo la kupata fikra mpya zitakazoiwezesha CCM kushinda katika
uchaguzi Mkuu wa 2020.
“Kwanza CCM inawapongeza Wilaya
ya Kaskazini “B” kupitia majimbo yenu mmefanya kazi nzuri katika Chaguzi
zote zilizopita chama kimeweza kushinda kwa ngazi mbali mbali na
kushika Dola.
Pia nakukumbusheni viongozi
muanze mapema kutoa taarifa kwa wanachama ili wapate muda mzuri wa
kujiandaa na uchaguzi huo wa chama ili kupata viongozi wenye uwezo
kiutendaji na kukabiliana na changamoto za kisiasa zilizopo Zanzibar, na
kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima.”, alifafanua Waride.
Aliwasihi viongozi wa Majimbo
wakiwemo wabunge , wawakilishi na madiwani kushirikiana na viongozi wa
Chama katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili
kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wananchi.
Aliwaagiza viongozi wa matawi
ndani ya wilaya hiyo kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujadili na
kubuni njia mbadala ya kuongeza wanachama wapya ndani ya chama ambao
ndio wapiga kura halali katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Naye Katibu wa Kamati Maalum
Idara ya Ogarnazesheni ya CCM Zanzibar, Haji Mkema alisema lengo lla
ziara hiyo ni kuwapongeza wanachama wa chama hicho na wananchi kwa
ujumla kwa kuichagua CCM kwa kura nyingi na hatimaye ikaongoza dola.
Aliwambia Makatibu wa Chama wa
ngazi mbali mbali ndani ya Wilaya hiyo kujenga utamaduni wa kuandaa
takwimu sahihi za wanachama kwa lengo la kujua ni wanachama wangapi
wamepungua na wameongezeka.
Mkema alisema wafuasi wa Chama
hicho wanatakiwa kufanya kazi za kuimarisha CCM , lakini pia watumie
fursa zinazowazunguka zikiwemo kilimo cha biashara na Chakula kujenga
uchumi wao.
“ Tufanye siasa kwa kuimarisha
chama chetu, lakini pia tunatakiwa kujenga uchumi wetu kwa kutumia fursa
zinazotuzunguka zikiwemo kilimo cha biashara kwani ardhi yetu ya Donge
ina historia ya rutuba kwa mazao mbali mbali hasa Karafuu.”, alishauri
Mkema.
Hata hivyo aliwataka wanachama
hao kujiunga na Jumuiya mbali mbali za CCM hasa za wanawake na vijana
ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali zinazopatikana kupitia jumuiya
hizo na kuweza kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wa wanachama wa chama
hicho waliiomba CCM kuendelea kuishauri serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza tatizo la ajira hasa
kwa vijana wanaoishi maeneo ya vijijini.
Aidha ameiomba serikali
kudhibiti vitendo vya uhamiaji holela ndani ya Wilaya hiyo kwani
unasababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kuibuka kwa tabia
zisizofaa katika jamii.
0 comments:
Post a Comment