Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limemfungia kwa kipindi kisichojulikana Msanii wa muziki wa kizazi
kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego hadi hapo
litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na Baraza
sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo
dhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Maagizo aliyopewa Msanii Nay ni
pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha Shilingi milioni 1, kufanya
marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata
sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya Sanaa kwa maana ya
kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.
Aidha, Msanii Nay ameagizwa
kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja maadili
na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususan wanawake.
Maamuzi haya yamefanyika kwa
mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984, ikisomwa
pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari, Utamaduni
na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Adhabu hizi zimetolewa kufuatia
BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu jana siku ya Jumanne
tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye kukiri makosa na
kuahidi kubadilika.
Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;
- Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.
- Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.
- Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.
Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yenye uvunjifu mkubwa wa maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha, tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako
wa Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya. Hivyo adhabu hii
imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama
kweli ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
0 comments:
Post a Comment